dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, May 16, 2018

Rais Magufuli aagiza mafuta ya kupikia yatolewe!

RAIS John Magufuli jana aliagiza kutolewa kwa tani 105,630 za mafuta ya kupikia yaliyo katika matangi ndani ya Bandari ya Dar es Salaam baada ya Mamlaka ya Mapato (TRA) kutoza kodi zinazostahili hata hivyo.Rais Magufuli alitoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kushtukiza kwenye Bandari ya Dar es Salaam, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema.

Akiwa katika ziara hiyo, taarifa hiyo ilisema zaidi Rais Magufuli aliiagiza TRA kutoza kodi zote stahiki na kuruhusu mafuta ya kupikia yaliyohifadhiwa katika matangi ya Kurasini kusambazwa, ili kuepusha upungufu unaoweza kujitokeza.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya kupokea ripoti ya timu ya uchunguzi juu ya uhalisia na ubora wa mafuta ya kupikia iliyoongozwa na Prof. Joseph Buchweishaija.

Taarifa kwa vyombo vya habari ilisema timu hiyo ilifanya uchunguzi katika matangi 43 yenye tani 105,630 za mafuta ya kupikia na kubaini kati ya matangi hayo, saba yalikuwa na mafuta yaliyoboreshwa.

Aidha, taarifa ilisema, matangi 14 yalikutwa na mafuta yaliyoboreshwa kiasi, manne yakiwa na mafuta ya kutengenezea sabuni na 18 yenye mafuta ghafi.

"Matokeo ya ripoti hiyo yameonesha kuwa, tofauti na taarifa zilizowasilishwa TRA na kampuni za uagizaji wa mafuta za Vegetable Oil Terminal(VOT), Tanzania Liquid Storage (TLS) na East Coast Oils and Fats Limited (EC) ambazo zilionesha sehemu kubwa ya mafuta hayo ni ghafi ambayo hutozwa kodi asilimia 10, imebainika kuwa kuna kiasi kikubwa cha mafuta yasiyo ghafi na ambayo yanapaswa kutozwa kodi asilimia 25," taarifa ilisema na kueleza zaidi:

"Kufuatia matokeo hayo Mhe. Rais Magufuli ameagiza mafuta yote yanayostahili kutozwa kodi ya asilimia 10 yatozwe hivyo, yanayostahili kutozwa kodi asilimia 25 yatozwe kwa kiwango hicho na wafanyabiashara wote waliofanya udanganyifu katika nyaraka kwa kuonesha kuwa mafuta yao ni ghafi wakati sio ghafi wapigwe faini kwa mujibu wa sheria na mafuta yaanze kusambazwa haraka iwezekanavyo.

"Mhe. Rais Magufuli amempongeza Prof. Buchweishaija na timu yake kwa kufanya uchunguzi wa kisayansi katika mafuta hayo, na pia amemtaka Mkemia Mkuu wa Serikali na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, ili kuondoa mianya ya wafanyabiashara wanaofanya hujuma dhidi ya uchumi na afya za Watanzania."

Aidha, taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli ameziagiza wizara za Fedha na Mipango na Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupeleka bungeni mabadiliko ya sheria za kodi za mafuta.

Lengo la mabadiliko hayo, taarifa ilisema Rais Magufuli amesema, ni kuondoa mianya ya ukwepaji wa kodi kwa waagizaji wa mafuta wanaodai mafuta ni ghafi wakati si kweli kwa lengo la kukwepa kulipa kodi halali za serikali.

“Nataka niwahakikishie Watanzania wote na ndugu zangu Waislamu mnaoanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, hakutakuwa na upungufu wa mafuta, na wanaofanya mchezo wa kutishia kuadimika kwa mafuta ili waachiwe kuingiza mafuta kwa kukwepa kodi hawataweza, nataka niwahakikishie serikali ipo makini,” taarifa ilimkariri Rais Magufuli akisema.

PONGEZA TRA
Wakati huo huo, taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Gerson Msigwa ilisema Rais Magufuli aliipongeza TRA kwa hatua ilizochukua kudhibiti wafanyabiashara waliotaka kukwepa kodi ya mafuta hayo.

Aidha, taarifa ilisema, alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James kumthibitisha Ben Asubisye kuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa TRA.

"Kabla ya kuondoka bandarini hapo Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage na Katibu Mkuu wake Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali nje ya Bandari ya Dar es Salaam na kuwaeleza kuwa serikali inachukua hatua za kudhibiti na kukabiliana na udanganyifu katika uagizaji wa mafuta, ili kuhakikisha wananchi wanakula mafuta salama, inakusanya kodi stahili na viwanda vya ndani ambavyo huzalisha ajira na kukuza uchumi wa nchi vinalindwa."

No comments :

Post a Comment