dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, November 11, 2018

CUF JUU YA: UTIAJI SAINI WA MKATABA WA UGAWANAJI FAIDA [PSA] BAINA YA ZANZIBAR NA KAMPUNI YA RAK GAS !


THE CIVIC UNITED FRONT

[CUF-CHAMA CHA WANANCHI]
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA UTIAJI SAINI WA MKATABA WA UGAWANAJI FAIDA [PSA] BAINA YA ZANZIBAR NA KAMPUNI YA RAK GAS YA RAS ALKHAIMAH 
TAREHE 11 NOVEMBER, 2018 

RAMADA ENCORE HOTEL DAR ES SALAAM:

1. UTANGULIZI
Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu [SW] kwa kutupa afya na kutuwezesha kukutana hapa leo, napenda kuwashkuru nyote mliohudhuria katika mkutano huu. Faida ya mkutano huu itapatikana kama hatimaye tutafikisha ujumbe wa mkutano huu kwa wananchi kwa ukamilifu na usahihi.

Hivi karibuni, tarehe 23 Oktoba 2018, tulishuhudia tukio la kihistoria la Zanzibar kutiliana saini na Kampuni ya Utafutaji na Uchimbaji Mafuta ya Rak Gas kutoka katika nchi ya Ras Alkhaimah ya taifa la Umoja wa Falme za Kiarabu [United Arab Emirates-UAE]. Mkataba uliotiwa saini ni kwa ajili ya kugawana faida itayopatikana pindipo uchimbaji wa mafuta au gesi utafanyika katika kitalu cha Zanzibar-Pemba [Production Sharing Agreement- PSA]. Kabla ya kutiwa saini mkataba huo, Kampuni ya Rak Gas iliajiri kampuni mbali mbali kwa ajili ya kufanya utafiti wa awali wa mafuta na gesi katika kitalu hicho. Utafiti huo ulihusisha wa angani na pia wa ardhini.

Suala la rasilimali ya mafuta na Gesi lina umuhimu wa aina ya pekee kwa Zanzibar na watu wake kutokana na mazingira ya kikatiba, kisheria na kiuchumi. Bila ya kuwepo umakini, ukweli wa dhati wa wanaolisimamia na uwazi, Zanzibar, watu wake na vizazi vyao vya baadae watajikuta wameingizwa katika mgogoro mwengine mkubwa sana sawa au zaidi ya ule mgogoro wa Mkataba wa Muungano. Hivyo, ni wajibu wa Wazanzibari wote kama inavyoelekezwa na Kifungu cha 23(4) cha Katiba ya Zanzibar kulivalia njuga jambo hili katika kulinda mamlaka ya Zanzibar na rasilimali zake.

Madhumuni makubwa ya Taarifa hii ni kuwatanabahisha Wazanzibari na Watanzania kwa jumla kwamba kwa kusainiwa Mkataba tulioutaja katika mazingira yaliyokosa umakini, yaliyojaa kutokujali Katiba wala sheria na maslahi mapana ya nchi na yenye utatanishi mkubwa na wa wazi wa kikatiba, kisheria na kisiasa, Zanzibar pamoja na vizazi vijavyo inaingizwa katika janga kubwa sana.


2. HISTORIA FUPI YA SUALA LA MAFUTA NA GESI KWA ZANZIBAR


Suala la Mafuta na Gesi kwa Zanzibar lina historia ndefu sana ambayo ni muhimu kujikumbusha japo kwa muhtasari:


a) Utafutaji wa mafuta na gesi kwa Zanzibar ulianza tokea miaka ya 1950 chini ya Sheria ya Madini ya Zanzibar Sura 106 ya mwaka 1925 ambayo ilirekebishwa mwaka 1951. Kampuni ya Mafuta ya Uingereza [British Petroleum- BP] iliongoza utafiti huo;


b) Mnamo mwaka 1968, Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Muda ya Muungano Namba 48 ya 1968, iliyaingiza mafuta yasiyochujwa na gesi kuwa mambo ya Muungano bila ridhaa wala mashauriano ya pande mbili za Muungano;


c) Mwaka 1996, Shirika la Maendeleo ya Mafuta la Serikali ya Muungano [TPDC] iliingia makubaliano na Kampuni ya Antrim ya Canada kwa ajili kuanza utafiti na uchimbaji mafuta katika kitalu cha Zanzibar-Pemba. Kampuni hiyo ilipotaka kuanza shughuli hizo Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilizuia kufanya hivyo kwa vile haikushauriwa wala kuombwa ruhusa na TPDC wala Serikali ya Muungano. Msimamo huo wa SMZ uliendelezwa katika miaka yote 10 ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Amani Karume;


d) Mwaka 2009, mbali ya kupitisha Sera ya Nishati ya Zanzibar, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa kauli moja lilipitisha azimio la kuitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuchukua hatua kwa kushirikiana na Serikali ya Muungano kuliondoa suala la Mafuta na Gesi katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Azimio hilo halijawahi kubadilishwa wala kufutwa;


e) Mwaka 2010 kampuni ya Rak Gas ilinunua hisa katika leseni ya Kampuni ya Antrim kuhusiana na kitalu cha Zanzibar-Pemba ambapo hatimaye ilinunua leseni na hisa zote katika kitalu hicho na hivyo kurithi ule mkataba wa Mgawano wa Faida [PSA] kutoka kwa Kampuni ya Antrim. Hivyo, si mara ya mwanzo wala siku ya mwanzo kwa kitalu hicho kufanyiwa makubaliano sawa na yale yaliyotiwa saini tarehe 23 Oktoba 2018. Makubaliano kama hayo yalishaingiwa miaka 22 iliyopita. Kilichobadilika tarehe 23 Oktoba ni watiaji saini, pahala na bila shaka karatasi za makubaliano hayo;


f) Mwaka 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha Sheria ya Mafuta [Petroleum Act] Namba 21 ya 2015. Upo ushahidi usio na shaka kwamba katika maandalizi yote ya awali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haikushirikishwa. Ilitakiwa maoni katika hatua za mwisho kabisa. Sheria hiyo sio tu kwamba iliimarisha udhibiti wa suala la mafuta na gesi kuwa chini ya Serikali ya Muungano, bali pia ili ilitanua mamlaka ya Serikali ya Muungano katika suala la mafuta na gesi na kwa mambo ambayo hata sio ya Muungano. Kwa mujibu wa Katiba ya Muungano mamlaka ya Serikali ya Muungano ni katika masuala ya utafutaji na uchimbaji tu [upstream], lakini chini ya Sheria hiyo, Serikali ya Muungano imejipa mamlaka hata katika maeneo ya uchakataji wa mafuta yasiyochujwa na usambazaji mafuta yaliyochujwa [mid-stream and down-stream]. Aidha, Sheria hiyo, iliiruhusu Zanzibar kuunda vyombo vyake yenyewe katika kusimamia utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi na pia kusimamia mapato yatayotokana na shughuli hizo;


g) Mwaka 2016, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha Sheria ya Mafuta ya Zanzibar ambayo kimaudhui haina tofauti na Sheria ya Mafuta iliyopitishwa na Bunge mwaka 2015. Mkataba uliotiwa saini tarehe 23 Oktoba ulitokana na kinachoitwa mamlaka ya SMZ chini ya Sheria hiyo ya Mafuta ya Zanzibar
Kutokana na mtiririko huo ulioelezwa hapo awali, ni Dhahiri kwamba uongozi uliopo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar umetia saini makubaliano hayo huku ikiwa bayana kwamba ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, kinyume na Sheria ya Mafuta iliyotungwa na Bunge, kinyume na Azimio la Baraza la Wawakilishi la mwaka 2009. Aidha, utiaji saini huo ni kinyume na msimamo na dhamira za Wazanzibari wote, msimamo na dhamira ambao ulisimamiwa kwa umakini mkubwa na viongozi wote waliotangulia ambao wote wametoka Chama cha Mapinduzi, tokea Dkt. Salmin Amour Juma na Dkt. Amani Karume pamoja na Ngome ya Wananchi wa Zanzibar, Baraza la Wawakilishi.
Utiaji saini mkataba huo ni wa historia iliyo mbaya kwa sababu Zanzibar imetoswa katika kiza kinene katika jambo nyeti, muhimu na linalogusa vizazi na vizazi vijavyo.
Tunayaeleza haya tukielewa kwamba katika utaratibu huu batili unaorasimishwa sasa hivi, katika mtindo wa Funika Kombe Mwanaharamu Apite, Serikali ya Muungano inaweza ikafumbia macho ubatili wote huo na kuiwachia Zanzibar itafute, ichimbe mafuta na ikusanye mapato yatayotokana na shughuli hizo. Tunachokizungumzia na ambacho wananchi wote wa Zanzibar na viongozi waliotangulia walikihofia ni kwamba utaratibu huo batili hauipi Zanzibar fursa endelevu na inayostahiki ya kuendeleza sekta yake ya mafuta na gesi katika kiwango na misingi itayovutia uwekezaji na itayoendana na viwango vya kimataifa vya usimamizi wa rasilimali zinazotokana na uchimbaji [extractive industry]. Kinachofanyika sasa ni sawa na kumpatia mgonjwa drip huku akisubiri matibabu. Lakini kinachosikitisha ni ile juhudi ya Watawala wa SMZ kutaka kuwaaminisha watu kwamba tayari mgonjwa ameshapatiwa matibabu na kwa hakika ameshapona- ilhali mgonjwa bado mahtuti na kila mtu anaona.
Tumelazimika kutoa maelezo haya ili kuzitanabahisha Serikali zote mbili kwamba juhudi hizi za kisanii za kulipamba suala la mafuta na gesi kuwa limeshapatiwa ufumbuzi baina ya Zanzibar na Tanzania Bara hazitasaidia na badala yake tunapanda mzizi mwengine mbaya zaidi wa fitna katika Muungano. Aidha, nia yetu ni kuwatanabahisha wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania Bara kwamba suala la kero ya mafuta na gesi baina ya Zanzibar na Serikali ya Muungano bado halijapatiwa ufumbuzi hata kidogo. Kinachofanyika sasa ni kufunika tatizo na kulirasimisha jambo ambalo litajenga mzizi wa fitna wa muda mrefu sana katika Muungano wetu.

3. KASORO ZA MSINGI AMBAZO HAZIJAPATIWA UFUMBUZI

Kama tulivyotangulia kueleza, kwa kutumia hatua ya utiaji saini mkataba wa ugawanaji faida, Uongozi wa Zanzibar unafanya juhudi kubwa ya kujisahaulisha na kutaka kuwasahaulisha Wazanzibari na Watanzania kwa jumla kwamba kero ya Muungano juu ya suala la mafuta na gesi halijapatiwa ufumbuzi na badala yake linarasimishwa na kutengenezwa kuwa gumu zaidi kulipatia ufumbuzi hapo siku za baadae. Kasoro za msingi ambazo hazijapatiwa majibu wala ufumbuzi ni kama zifuatazo:


a) Kasoro ya Kikatiba:
Ukweli kwamba suala la mafuta na gesi bado limo katika Orodha ya Mambo ya Muungano chini ya Jadweli la Kwanza la Katiba halina mjadala. Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza bayana na kwa lugha fasaha sana kwamba jambo likiwa limo katika Orodha ya Muungano, basi jambo hilo limo katika mamlaka ya Serikali ya Muungano. Ibara ya 34(1) inaeleza kama ifuatavyo:
“Kutakuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na mamlaka juu ya MAMBO YOTE YA MUUNGANO katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo yote yahusuyo Tanzania Bara”
Aidha, kwamba ibara ya 64(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inabatilisha Sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi kwa jambo ambalo ni la Muungano kwa maelekezo yasiyo na utatanishi, pia halina mjadala. Ibara hiyo ya 64(3) inaelekeza ifuatavyo: “Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa batili na itatenguka…
Kutokana na maelekezo hayo ya wazi ya Katiba, ni dhahiri kabisa kwamba Sheria ya Kusimamia Mafuta na Gesi, Namba 6 ya 2016 iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi inapingana moja kwa moja na masharti ya ibara ya 64(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Ingawa tunafahamu kwamba utawala uliopo wa Zanzibar haujali Katiba wala haukerwi na ubatili wowote ule katika vitendo na uendeshaji wao wa shughuli za umma, lakini kutokujali ubatili wa kiwango hichi na ambao unahusu suala nyeti la kikatiba, kiuchumi na kimustakbala wa nchi yetu ni wa kiwango kilichopitiliza mipaka yote na inaweza kuiingiza nchi yetu katika hasara kubwa sana badala ya faida.
Ukweli kwamba mkataba huo umesainiwa na Kampuni inayomilikiwa na Ras Alkhaimah, moja ya nchi iliyomo katika Muungano wa Falme za Kiarabu [United Arab Emirates] ingetosha kuwasuta nakuwatanabahisha watawala wa Zanzibar kwamba hivi imeshindikana kitu gani kwa Zanzibar kuwa na uhuru wa kusimamia rasilimali yake ya mafuta na gesi kama Ras Alkhaimaha. Ni ushuhuda kwamba kama kweli nia njema ipo baina ya pande mbili za Muungano, suala la kurekebisha Katiba kuondoa ubatili uliopo lilipaswa liwe jambo la kipaombele na rahisi. Chini ya Muungano wa Falme za Kiarabu kila nchi shiriki katika Muungano wao ipo huru kusimamia rasilimali yake ya mafuta na gesi kwa kadri inavyopenda. Ni aibu na fedheha kubwa kwa Dr Ali Mohamed Shein kueleza mbele ya kadamnasi ya watu kwamba utiaji saini huo umewezekana baada ya kupewa ruhusa na Serikali ya Muungano na kwa ihsani kubwa ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Rais Dr John Pombe Magufuli. Tulitarajia angetanabahi kwamba upande wa pili wa mkataba nao wamo katika Muungano lakini haukusaini mkataba huo kwa kuruhusiwa na Abudhabi wala kwa ihsani ya mtu yeyote, bali kwa umadhubuti wa mfumo wao wa Muungano ambao unatoa fursa kwa kila nchi shiriki kufanya shughuli zao za kiuchumi bila vikwazo. Tulitarajia katika hafla ile, badala ya kuendeleza ubatili na kupalilia mgogoro wa kikatiba, kauli thabiti ya kupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro huo wa kikatiba ingetolewa na kutekelezwa ipasavyo.

b) Kasoro na Mgongano wa Kisheria
Kama tulivyotangulia kueleza kwamba Sheria ya Mafuta ya 2015 iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano imeeleza wazi katika kifungu cha 2 kwamba Sheria hiyo ndiyo itayotumika katika kusimamia masuala yote ya mafuta na gesi katika ngazi zote tatu [Upstream, Midstream na Down-Stream]. Kifungu hicho cha 2 kimeeleza bayana kwamba shughuli hizo zitapofanyika Tanzania Bara zitasimamiwa na vyombo vilivyoanzishwa au kutambuliwa na Sheria hiyo. Na shughuli hizo zitapofanyika Zanzibar zitasimamiwa na vyombo vilivyoanzishwa chini ya Sheria za Zanzibar. Kifungu hicho kinaeleza ifutavyo:
2.(1) This Act shall, subject to subsection (2) apply to Mainland Tanzania as well as Tanzania Zanzibar-
(2) The regulation of petroleum upstream operations, midstream and downstream activities and matters incidental thereto to which this Act apply shall-
(a) where such operations or activities are undertaken within Mainland Tanzania, be governed and administered by institutions established or referred to under this Act; and
(b) where such operations or activities are undertaken within Tanzania Zanzibar, be governed and administered by institutions in accordance with the laws of Tanzania Zanzibar.
Haihitaji utaalamu wa sheria kufahamu kwamba Sheria hiyo imeiruhusu Zanzibar kuanzisha vyombo vya kusimamia Sheria hiyo iliyotungwa na Bunge kwa upande wa Zanzibar. Badala ya kuanzisha vyombo vya kusimamia Sheria hiyo ya Mafuta, Zanzibar nayo ilitunga Sheria nyengine ya Mafuta na Gesi Namba 6 ya 2016 [Oil and Gas (Upstream) Act]. Huu ni mgongano wa wazi wa kisheria ambao unatishia kutokea matatizo makubwa hapo baadae.
Mgongano huu wa kisheria ukichanganya na mgogoro wa kikatiba una athari kubwa sana. Miongoni mwa athari hizo ni kama zifuatazo:
i. Nani mmiliki wa mafuta na gesi- Zanzibar au Tanzania: kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mafuta 2015 ya Tanzania inaeleza bayana nani mmiliki wa mafuta na gesi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maneno yafuatayo:
“4.-(1) The entire property in and control over petroleum in any land to which this act apply are vested in the United Republic and shall be exclusively managed by the Government on behalf of and in trust for the people of Tanzania, but without prejudice to any right to explore, develop or produce petroleum granted, conferred, acquired or served under this act or the relevant law Tanzania Zanzibar.


Kwa mujibu wa kifungu hicho ni wazi na dhahiri kwamba mwenye hati miliki ya rasilimali ya mafuta na gesi katika Tanzania ni Jamhuri ya Muungano. Aidha, kwa maneno fasaha na bayana ilichopewa Zanzibar ni haki ya kutafuta, kuendeleza na kuzalisha mafuta na sio hati miliki ya mafuta na gesi. Kwa ufupi walichopewa Zanzibar ni sawa na haki ya matumizi au sawa na mpangaji mwenye haki ya matumizi lakini hana haki ya umiliki.


Kwa upande mwengine kifungu cha 4 cha Sheria ya Zanzibar kinaipa hati miliki ya mafuta na gesi Zanzibar kinyume kabisa na yaliyoelezwa na Sheria ya Tanzania. Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Zanzibar kinaeleza ifuatavyo:
“Subject to the provisions of this Act, the entire property in, and the control of petroleum in its natural condition in, on or under any land or territorial waters in Zanzibar and derived from any international laws is vested in the Government on behalf of the people of Zanzibar”

Ni aibu kubwa sana ama ni udanganyifu wa hali ya juu sana unaofanywa na watawala wa Zanzibar kujimilikisha jambo ambalo ni wazi kwamba hawakupewa mamlaka ya kikatiba na kisheria. Ni fedheha kubwa zaidi kusimama mbele ya raia na kuwadanganya kwamba Zanzibar ina mamlaka yote wakati haina hata umiliki wa rasilimali ya mafuta na gesi wakati Katiba na Sheria ya Muungano inaeleza bayana kwamba Zanzibar haijapewa mamlaka hayo.
Kibaya zaidi ni kwamba mgongano huu wa wazi wa sheria unapanda mbegu ya uhasama mkubwa hasa itapotokea rasilimali hiyo ikigundulika kwa wingi sana Zanzibar.


ii. Mgawano na Utambuzi wa Vitalu: Katika utafutaji na uchimbaji wa mafuta jambo la mwanzo kabla ya yote ni kueleweka mipaka ya maeneo ya kila mamlaka inayosimamia utafutaji na uchimbaji mafuta. Hili ni muhimu ili kuepusha migogoro. Mfano mzuri kwa muda mrefu kumekuwepo na tatizo la uvuvi katika bahari ya Tanzania [territorial sea] kwa vile zipo mamlaka mbili za leseni. Wavuvi kutoka pande mbili za Muungano, na hasa wale wanaotoka Zanzibar wamekuwa wakipata usumbufu wa kukamatwa na maafisa wa uvuvi wa Tanzania Bara wakati bado wapo katika mipaka ya bahari ya Zanzibar.
Katika hili la utambuzi na ugawaji wa vitalu tayari tatizo la msingi linajitokeza na ambalo lazima lipatiwe majibu. Kwa mfano kitalu cha Zanzibar Pemba ambacho mkataba wake ulitiwa saini tarehe 23 Oktoba, kimeingia hadi maeneo ya bahari na nchi kavu ya Tanzania Bara. Kwa vile kifungu cha 4 cha Sheria ya Mafuta ya 2015 kinaeleza kwamba mamlaka ya vyombo vya Zanzibar ni kwa maeneo ya kijiografia ya Zanzibar, suala ni kwamba jee kitalu hicho ni cha Zanzibar au ni cha pamoja au ni kitalu kilichoingiliana [overlapping block]. Kama ni kitalu cha pamoja bila shaka pande zote zilipaswa kutia saini, kama kimeingiliana, sheria imeweka utaratibu maalumu katika kushughulikia vitalu vilivyoingiliana. Katika hili hakuna majibu ya wazi.


Suala jengine lenye mgogoro wa wazi ni kwamba hadi sasa ni vipi vitalu vya Zanzibar katika eneo la bahari kuu [off-shore blocks]. Imani iliyopo ni kwamba vitalu namba 9 hadi 12 ni vya Zanzibar lakini hakuna sheria wala muongozo ulioweka wazi jambo hilo. Aidha, hadi sasa suala la vitalu namba 7 na 8 ambavyo tayari vilishagaiwa na TPDC na kuwapa Kampuni ya Petrobras bado lina mgogoro mkubwa kutokana na vitalu hivyo kuingia katika eneo la Zanzibar likiwemo la kisiwa cha Fungu Mbaraka [Latham Island].
Hadi sasa, utawala wa Zanzibar unakwepa kujibu suala hilo hata lilipoulizwa katika Baraza la Wawakilishi.


iii. Mamlaka ipi ina uwezo wa kugawa vitalu: Mgogoro wa kikatiba na kisheria unazusha hoja moja muhimu sana nayo ni kwamba ni nani mwenye mamlaka ya kugawa vitalu. Hili ni jambo muhimu sana na ambalo halina majibu katika Sheria zote mbili. Kwa mujibu wa kifungu cha 33 cha Sheria ya Mafuta ya Zanzibar mamlaka ya kugawa vitalu ipo kwa Waziri anayehusika na mafuta na gesi wa Zanzibar. Wakati kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya 2015 iliyopitishwa na Bunge kifungu cha 32 kinatoa mamlaka ya kugawa vitalu kwa Waziri wa Nishati wa Serikali ya Muungano. Kutokana na kukosekana mipaka ya pande mbili za Muungano kwa madhumuni ya shughuli za mafuta na gesi, vifungu hivyo viwili vinaleta mzozo mkubwa juu ya nani mwenye mamlaka ya kugawa vitalu. Jambo baya zaidi ni kwamba sheria zote mbili hazikuweka utaratibu wa kutatua mzozo unapotokea baina ya pande mbili za Muungano katika suala la mafuta na gesi. Bila shaka kutokuwepo uwazi huo kunaipa nguvu Serikali ya Muungano kutumia nguvu zake za kikatiba na hata za kisheria kuiburuza Zanzibar kama inavyoendelea kufanyika sasa hivi.

c) Kukosekana Uwazi
Mafuta na gesi ni rasilimali za wananchi wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mafuta ya Zanzibar imeeleza wazi kwamba rasilimali ya mafuta na gesi ni mali ya Wananchi wa Zanzibar ambayo Serikali inakabidhiwa kuisimamia na kuiendesha kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar. Kwa sababu hiyo, Serikali inatakiwa iweke bayana mambo yote muhimu katika suala la mafuta na gesi na hasa mikataba inayotiwa saini.
Miongoni mwa nguzo kuu za shughuli za uchumi wa gesi na mafuta ni uwazi [transparency]. Ni kutokana na umuhimu wa uwazi ndio maana mataifa yaliungana kuanzisha mpango maalumu wa uwazi katika sekta ya shughuli za uchimbaji [extractive industry]. Mpango huo unaojulikana kama Extractive Industries Transparency Initiative [EITI] ambao makao makuu ya Sekretariati yake ni Norway, unasimamia masuala yote ya utawala bora na uwazi katika sekta hiyo. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijiunga na mpango huo mwaka 2009 na mwaka 2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likatunga Sheria ya kuanzisha mpango huo kwa Tanzania [Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative- TEITI]. Kwa mujibu wa Ripoti ya TEITI ya mwaka 2015/16 ambayo imetolewa mwezi March 2018, Tanzania tokea ijiunge na mpango huo wa uwazi imeshatoa Ripoti 7 za uwazi ambazo zinaonyesha kwamba kati ya mwaka 2008 hadi 2015 Serikali imekusanya mapato ya Dola za Marekani bilioni 2.7/ katika sekta ya uchimbaji kwa jumla.
Aidha, katika kuendeleza uwazi, mwaka 2017, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilifanya marekebisho ya Sheria ya Mafuta ya 2015. Miongoni mwa marekebisho hayo, kifungu cha 47 kimerekebishwa ili kuweka uwazi zaidi katika mikataba ya mafuta. Kifungu hicho sasa kinaeleza:

(6) Notwithstanding the provisions of this Act and any other written law, the agreement under subsection (1) shall only enter into force upon approval by the National Assembly.”

Katika suala la mafuta na gesi, utawala wa SMZ unalifanya kwa usiri usioendana na viwango vya ndani na vile vya kimataifa. Tulitarajia kwamba baada ya Bunge kuonesha njia, na utawala wa SMZ nao ungelishirikisha Baraza la Wawakilishi katika kuidhinisha mkataba huo kama inavyotakiwa na Sera ya Nishati ya Zanzibar ya 2009.
Hadi sasa mbali ya taarifa ya sherehe, utawala wa SMZ hauwapi wananchi fursa ya kufahamu kwa kina kinachoendelea, kinachofuata na matarajio ya baadae. Hii ni kasoro kubwa sana.
Kwa ujumla kasoro hizo zote zinafanya suala nyeti la uchumi wa mafuta na gesi kuwa na wingu kubwa badala ya kuwa na mwanga wa matumaini kwa maendeleo ya wanachi na Zanzibar kwa ujumla.
Kasoro hizo, ukichanganya udhaifu mkubwa na wazi ulioonyeshwa na utawala uliopo wa Zanzibar katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita katika kusimamia maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano kunaleta fadhaa na masikitiko makubwa kwa wananchi wa Zanzibar. Kunawafanya wananchi wapoteze matumaini kwamba rasilimali nyeti ya mafuta na gesi inasimamiwa katika mtindo wa shaghalabaghala jambo linaloiweka hatma ya Zanzibar katika majaribu makubwa.

4. HITIMISHO
Tunapenda kukumbusha na kutanabahisha kwamba Chama cha Wananchi [CUF] ndicho kilichokuwa cha mwanzo kuweka bayana uono wake, sera na msimamo juu ya suala la uchumi wa mafuta na gesi Zanzibar. Wakati CUF ikiweka bayana mikakati hiyo, CCM Zanzibar na viongozi wake walikejeli sana mkakati huo wakiziita ni ndoto za mchana. Wao hawakuwa na uono, sera wa msimamo juu ya suala hilo. Tunashukuru kwamba kweli ikidhihiri, uongo hujitenga. Ilipodhihiri kwamba kweli rasilimali ya mafuta na gesi ipo Zanzibar, viongozi waliotangulia waliweka msimamo ambao ulijenga matumaini makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Matumaini hayo yameyeyushwa na udhaifu na kukosa maono na ujasiri kwa utawala uliopo sasa hivi wa Zanzibar. Hivyo, tunaeleza haya kwa masikitiko makubwa sana na kwa nia ya kuungana na wananchi wa Zanzibar katika kueleza na kuendelea kutanabahisha kwamba utawala uliopo sasa usilifanye suala la mafuta na gesi kuwa la mpito wala la siasa. Suala hili ni la muda mrefu na kwa faida ya vizazi vijavyo. Jambo hili ni la maslahi mapana ya nchi na mustakbala wake na sio la siasa au la awamu za uongozi.
Tumeyaeleza haya yote si kwa nia ya kukwamisha, kuhujumu, kurudisha nyuma wala kuzorotesha hatua zozote zile za kuendeleza suala la mafuta na gesi kwa sababu sisi tunaamini kwamba ni waanzilishi na wadau muhimu wa juhudi hizo. Tutachoendelea kukisimamia kwa nguvu zetu zote ni kuona kwamba suala la gesi na mafuta linaendeshwa kwa misingi inayokubalika kikatiba, kisheria na kiutawala kwani tunaamini ni kwa kuzingatia misingi hiyo pekee ndipo suala hilo litakuwa endelevu, litavutia uwekezaji na litakuwa na tija kwa wananchi wa Zanzibar na watu wake. Ubabaishaji na usanii huu unaofanywa na utawala wa sasa wa Zanzibar ni kuwadanganya wananchi kwa manufaa binafsi na manufaa ya kisiasa yasiyo endelevu ambao yanaikosesha Zanzibar fursa adhimu ya kujikwamua katika umaskini ulifurutu ada.
Bila ya shaka ndani ya ubatili huu wa sasa faida na manufaa yanaweza kupatikana na sisi tunakaribisha faida na manufaa hayo, lakini faida na manufaa hayo hayatakua yanaakisi malengo ya Zanzibar na hayatakuwa na wigo stahiki wa fursa ziliopo katika uchumi wa mafuta na gesi kwa Zanzbar. Tunaisihi Serikali ya Muungano na hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dkt John Pombe Magufuli kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala la mgogoro wa kikatiba na kisheria katika mafuta na gesi ili kujenga mustakbala imara wa uchumi wa mafuta na gesi kwa Tanzania. Sasa hivi ana fursa adhimu na pekee ya “kuitumbua” kero hii na Zanzibar na Tanzania itamkumbuka milele kama bingwa wa kutumbua kero iwapo ataipatia ufumbuzi wa kudumu kero hii ambayo inahatarisha amani, utulivu na maelewano baina ya pande mbili za Muungano.

HAKI SAWA KWA WOTE



MAALIM SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU.THE CIVIC UNITED FRONT
[CUF-CHAMA CHA WANANCHI]

No comments :

Post a Comment