Na Hellen Mwango
Wanamuziki,Nguza Vicking maarufu kama 'Babu Seya'na mwanawe Papii
Nguza au Papii Kocha(Kushoto),wakiwaaga ndugu,jamaa,marafiki,wanamuziki na
wapenzi wao wakati wakirudisha gerezani,baada ya Mahakama ya Rufani jijini Dar
es Salaam jana,kukataa ombi lao la kupitia upya hukumu ya kifungo cha maisha
jela dhidi yao.
Kadhalika, mashabiki wa wanamuziki hao waliokuwa wamefurika katika viunga hivyo, kila mmoja alionekana akishindwa kujizuia kumwaga machozi baada ya Msajili wa Mahakama hiyo, Zahara Maluma, kumaliza kusoma uamuzi wa mapitio ya hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo Februari 11, 2010.
Saa 5:05 asubuhi ukumbi namba moja wa mahakama hiyo ulifurika watu wakiwamo wanamuziki, ndugu, marafiki, wanahabari na wanasheria kusikiliza uamuzi wa mapitio na Maluma baada ya jopo la majaji watatu kusikiliza mapitio hayo, Oktoba 30, mwaka huu.
Jopo hilo liliongozwa na Mwenyekiti Nathalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk na Salum Massati ambao pia walisikiliza maombi ya rufaa ilipofunguliwa mahakamani hapo.
Maluma alisema mahakama imetupa maombi ya Babu Seya na mwanae Papii Nguza maarufu kama Papii Kocha na kwamba ilikuwa sahihi katika hukumu yake ya awali ya kuwaona wana hatia ya kuendelea kutumikia adhabu hiyo.
Alisema kwa mujibu wa jopo lililosikiliza mapitio hayo, hoja zilizotolewa na Babu Seya na mwanae kuhusu mahakama hiyo kuteleza na kuwaona bado wana hatia hazina mashiko ya kisheria na kwamba jopo hilo lilikuwa sahihi mwanamuziki huyo na mwanae wana hatia ya makosa matano ya kubaka kati ya makosa 23 yaliyokuwa yanawakabili yakiwamo ya kulawiti wanafunzi wa shule ya msingi.
Alisema hoja za Babu Seya na mwanae kupitia wakili wao, Mabere Marando za kuitaka mahakama hiyo kuwaachia huru hazina msingi wa kisheria na adhabu yao itaendelea kama ilivyoamriwa awali na mahakama hiyo.
Baada ya kumaliza kusoma uamuzi huo, Babu Seya aliyekuwa amevaa shati lenye mchanganyiko wa maua ya rangi ya bluu na nyeusi, suruali nyeusi na viatu maarufu kama mokasini nyeusi, alitikisa kichwa akiwa ndani ya kizimba cha mahakama hiyo huku mwanae akiwa amejiinamia chini.
Aidha, ndugu, jamaa na majirani walitoka nje ya ukumbi huo huku wakilia na wengine walionekana kuzungumza na simu.
NIPASHE ilihoji watu mbalimbali wakiwamo wanasheria ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini.
“Hapo hakuna jinsi tena labda waombe full bench (jopo la majaji watano), lakini sheria imeshachukua mkondo wake,” alisema wakili huyo Mwandamizi na mwingine aliongeza.
“Hatua ya leo (jana) ni ya mwisho hata hao wanaosema kwamba labda Rais awahurumie, lakini hana mamlaka ya kuingilia sheria hasa kwa makosa waliyotenda Babu Seya na mwanae, adhabu yao hawezi kuingilia kabisa pamoja na kwamba ni mkuu wanchi.”
Jose Mara, mwanamuziki wa bendi ya Mapacha Watatu, alisema hakutegemea kama Babu Seya atarudi tena gerezani kwa kuwa alikuwa na matumaini makubwa ya kurudi naye uraiani kuendeleza muziki wa bongo.
“Kwa sababu kuna mahakama ambayo inasimamia misingi ya sheria, hatuna budi kukubali hali iliyotokea kwa baba yetu Babu Seya na ndugu yetu Papii Kocha,” alisema Mara.
Bahati Ally, alisema kilio chake kikubwa ilikuwa ni kumuomba Mungu Papii Kocha aachiwe huru kwa sababu walifanya kazi kwenye bendi ya FM Academia kwa ushirikiano mkubwa.
Naye wakili wao, Gabriel Mnyele, alisema hawana budi kukubali maamuzi ya mahakama kwa kuwa ni ya kisheria na hakuna aliye juu ya sheria.
Februari 11, mwaka 2010 mahakama hiyo iliwaachia huru watoto wawili wa Babu Seya, Nguza Machine na Francis Nguza baada ya kuwaona hakuna ushahidi ulioonyesha kwamba wana hatia katika makosa hayo Hata hivyo, iliwaona Babu Seya na Papii Nguza wana hatia ya makosa matano ya kubaka kati ya makosa 23 yaliyokuwa yanawakabili yakiwamo ya kulawiti hivyo aliwasilisha maombi mahakamani hapo ya kufanya mapitio.
Oktoba 30, mwaka huu mahakama hiyo iliyoketi chini ya jopo la majaji Kimaro, Mbarouk na Massati ilisikiliza hoja za pande zote mbili kuhusu mapitio hayo.
Katika hoja zao kupitia wakili Mabere Marando, Babu Seya na Papii Kocha aliiomba mahakama kuwaachia huru wanamuziki hao wanaotumikia kifungo cha maisha kwa makosa ya kulawiti na kubaka kutokana na ushahidi uliotumika kuwatia hatiani kuwa na mapungufu ya kisheria.
Kadhalika, alidai kuwa mahakama hiyo ikijielekeza kwenye ushahidi uliotolewa na baadhi ya mashahidi wa Jamhuri kwamba haukufuata masharti ya sheria ya kupokea ushahidi wa watoto wadogo ni rai ya upande wa utetezi itupilie mbali na kuwafutia warufani mashitaka yaliyowatia hatini.
Alidai lengo la kufikisha maombi hayo mahakamani hapo ni kuitaka kupitia makosa yanayojionyesha kuonyesha kwamba mahakama hiyo iliteleza bila kuwaachia warufani na badala yake ilitumia ushahidi wa watoto ambao ulikuwa na mapungufu ya kisheria.
Alidai kuwa mbali na mapungufu hayo pia, upande wa Jamhuri haukuita mashahidi muhimu kwenye kesi hiyo ambao walitajwa na baadhi ya mashahidi akiwemo Mangi mwenye duka jirani na nyumba ya Babu Seya.
Alidai kuwa kama Mangi angeitwa mahakamani na angeweza ukweli kinyume na ushahidi wa Jamhuri, hivyo kwa kuwa waliona atawaharibia kesi yao wakaamua kumuacha kwa makusudi.
Aliendelea kudai kuwa pia kuna kijana mwingine Zizeli aliyetajwa katika ushahidi kwamba alikuwa akikusanya watoto kwa ajili ya kuwapeleka kwa warufani hao, hajaitwa mahakamani kuthibitisha tuhuma hizo.
Alidai kuwa ushahidi huru uliotumika kuunga mkono ushahidi wa watoto uliotumika kuwatia hatiani Babu Seya na mwanawe, taratibu za kisheria zilikiukwa upande wa utetezi uliomba mahakama kuwaachia huru warufani hao.
Upande wa Jamhuri uliokuwa na jopo la mawakili watano, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Jackson Mdaki akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Angaza Mwipopo, Immaculate Banzi, Joseph Pande na Wakili wa Serikali Abrimark Mabruki.
Mdaki alidai kuwa maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi hayana mashiko ya kisheria kwa sababu kifungu kilichotumika kuyafungua mahakamani hapo ni cha mashauri ya madai na siyo ya Jinai kama kesi hiyo iliyopo mahakamani.
Aliiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo na kwamba kukubali kuyasikiliza na kuyatolea maamuzi ni sawa na matumizi mabaya ya mahakama huku akiongeza kuwa maombi hayo yalifunguliwa chini ya kifungu cha mashauri ya madai na siyo kesi za jinai.
Mwaka 2010 mahakama hiyo iliwaona Babu Seya na mwanae mmoja Papii Nguza wana hatia ya makosa matano ya kubaka kati ya makosa 23 yaliyokuwa yanawakabili yakiwemo ya kulawiti.
Hukumu hiyo ilisomwa na Msajili wa Mahakama hiyo, Neema Chusi, baada ya kusikilizwa na jopo hilo la majaji.
Alisema jopo hilo baada ya kupitia hoja hizo liliwaona Babu Seya na Papii hawana hatia katika makosa 18 yakiwamo ya kubaka na kulawiti.
Msajili Chusi alisema katika hati ya mshitaka kulikuwa na mapungufu kwa jina la shahidi Amina Shomari ambalo sehemu nyingine liliandikwa kwa kifupi A S.
Alisema pamoja na mapungufu hayo, Hakimu Addy Lyamuya aliyesikiliza kesi hiyo katika Mhakama ya Kisutu hakuamuru upande wa mashitaka kubadilisha hati hiyo huku akijua ina mapungufu ya kisheria na kutoa hukumu dhidi ya washitakiwa hao bila kuzingatia kasoro hizo.
Aidha pamoja na mapungufu hayo, baada ya kuwafutia makosa 18, mahakama hiyo ilimtia Babu Seya hatiani katika makosa ya ubakaji na Papii makosa mawili ya ubakaji.
Desemba, mwaka 2009, Mahakama hiyo iliyokuwa imeketi chini ya jopo la majaji watatu, ilisikiliza rufaa hiyo kupinga uamuzi ulikuwa umetolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Aidha, mahakama hiyo, iliambiwa kwamba Hakimu Lyamuya aliongeza maoni yake katika kutoa adhabu ya kifungo cha maisha kwa kama Babu Seya na wanawe watatu,badala ya kufuata utaratibu wa kisheria.
Marando aliomba mahakama hiyo kuwaachia huru wateja wake hao kwa kuwa ushahidi uliotumika kuwafunga ulikuwa na mapungufu ya kisheria.
Pia, aliiambia mahakama kuwa, watoto tisa kati ya 10 waliotoa ushahidi katika kesi hiyo hawakuapishwa na mahakama hatua ambayo ni kinyume cha sheria.
Juni, mwaka 2004, Mahakama ya Kisutu ilimhukumu Babu Seya na wanawe walihukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo hicho baada ya kukutwa na hatia ya makosa 10 ya kubaka watoto wa kike wenye umri kati ya miaka sita na minane na makosa mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri huo huo.
Hata hivyo, Januari 27, 2005, waliwasilisha rufaa kupinga adhabu hiyo katika Mahakama Kuu kupitia kwa Jaji Thomas Mihayo ambaye hata hivyo aliitupilia mbali rufaa yao ya awali iliyofunguliwa na wakili wao, Herbert Nyange.
Katika mashitaka yao, washitakiwa kwa pamoja walidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili na Oktoba 2003 maeneo ya Sinza Jijini Dar es Salaam.
Mbali na Machine na Francis, mwalimu wa shule ya Msingi ya Mashujaa, Sigirinda Ligomboka, alishtakiwa kwa makosa mawili ya kumsaidia Babu Seya kutenda makosa ya kubaka na kulawiti kwa kuwaruhusu baadhi ya watoto hao kutoka madarasani.
Hata hivyo, Lyamuya alimuachia huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Baada ya mahakama hiyo kutoa uamuzi huo, Babu Seya na mwanae walirejeshwa gerezani huku wakiwapungia mikono ndugu, jamaa, marafiki na wanamuziki wenzao waliokuwapo mahakamani hapo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment