Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa uwasilishaji wa utafiti uliofanywa na taasisi yake kuhusu mtazamo wa wazazi juu ya lugha gani itumike kufundishia shuleni. Katikati ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora wa Elimu nchini, Marystella Wassena na Profesa Kitila Mkumbo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Picha na Venance Nestory.
- Watu 1,381 kutoka Tanzania Bara pekee walihojiwa katika utafiti huo uliofanywa kwa njia ya simu za mkononi. Pia, watu waliohojiwa wana viwango tofauti vya elimu kuanzia darasa la saba mpaka elimu ya juu.
Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza umebaini kuwa watu sita kati ya 10 wangependa Kiingereza kiwe lugha ya kufundishia katika shule za msingi na sekondari, wakati Sera ya Elimu iliyozinduliwa mwaka huu inaruhusu matumizi ya lugha hiyo sambamba na Kiswahili.
Watu 1,381 kutoka Tanzania Bara pekee walihojiwa katika utafiti huo uliofanywa kwa njia ya simu za mkononi. Pia, watu waliohojiwa wana viwango tofauti vya elimu kuanzia darasa la saba mpaka elimu ya juu.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mshauri wa Twaweza, Profesa Kitila Mkumbo alisema asilimia 63 ya waliohojiwa walisema wanataka watoto wao wafundishwe kwa lugha ya Kiingereza kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Profesa Mkumbo alisema wazazi wa watoto walisema kubadili lugha kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza kunasababisha matatizo.
Alisema asilimia 89 ya wazazi hao walikubali kuwa kuna changamoto, huku asilimia 10 wakisema hakuna matatizo.
“Asilimia 65 ya wazazi walisema watoto wao walimaliza elimu ya msingi, asilimia 26 walisema watoto wao walimaliza elimu ya sekondari na asilimia 8 walikuwa na watoto waliosoma elimu ya juu,” alisema Profesa Mkumbo.
Walipoulizwa kuhusu ubora wa elimu ya msingi, asilimia 64 ya wazazi walikubali kuwa ni bora, asilimia 62 ya wazazi wenye elimu ya sekondari walisema iko vizuri na asilimia 50 ya wahitimu wa elimu ya juu walisema elimu ya msingi ni nzuri.
“Hapa utagundua kuwa elimu aliyonayo mzazi pia inasaidia katika kufanya maamuzi sahihi. Hiyo asilimia 64 waliosema elimu ya msingi ni nzuri, wao pia wana elimu hiyo, kwa hiyo wengi wao pia hawana ujuzi wa upeo mkubwa,” alisema.
Matarajio ya wazazi hao pia yalikuwa tofauti wengi, wakitaka watoto wao wafanye kazi za udaktari na ualimu.
“Asilimia 2 tu walisema wangependa kuona watoto wao wakijikita kwenye kilimo ambacho wengi wanakitegemea,” alisema.
Mkurugenzi wa ukaguzi na udhibiti wa shule nchini, Marystella Wasena alikiri kuwa kuna shida kubwa katika kuchagua lugha ya kufundishia.
Alisema mtu akitumia lugha ambayo haijui vizuri atashindwa kujiamini na kufanya jambo la maana.
Alisema ni jukumu la kila mmoja kutafakari namna ya kulitoa Taifa katika mkanganyiko uliopo kwa lengo la kumpa mwanafunzi elimu ambayo itakuwa na athari chanya kwenye jamii anayotoka.
“Inawezekana mitalaa yetu iko vizuri, lakini namna inavyotolewa ikawa ndiyo tatizo. Sera ya elimu ni nyumbufu (flexible), imetoa uhuru wa kutumia lugha ya Kiswahili au Kiingereza kama lugha ya kufundishia,” alisema mkurugenzi huyo. Alisisitiza kuwa watu wasiangalie matumizi ya lugha ya Kiswahili pekee, bali waonyeshe na mapungufu mengine kama vile mitalaa, namna elimu inavyotolewa au wingi wa wanafunzi shuleni.
Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh aliyehudhuria hafla ya kutangazwa kwa matokeo ya utafiti huo, alisema hakuna namna yoyote nchi hii inaweza kukwepa matumizi ya lugha mbili.
“Sera ya elimu iko very clear (wazi), inatoa uhuru wa kutumia lugha zote mbili kwa wakati mmoja. Hata nchi nyingine pia zinafanya hivyo. Kwa hiyo tusiibeze sera ya elimu. Jambo la msingi ni kusimamia utoaji wa elimu hii,” alisema.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment