Mjadala mkali ilizuka kati ya vyama vya siasa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), juu ya kusainiwa mwongozo wa maadili ya uchaguzi mkuu.
Hoja mbalimbali zilijadiliwa kwa takribani saa nane huku vyama vya siasa vya upinzani vikigoma kusaini kwa madai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikacha kikao hicho.
Vyama vyote viliteua mwakilishi aliyehudhuria kikao hicho isipokuwa CCM.
“Kama tunataka kujenga mustakabali mzuri katika uchaguzi mkuu ni lazima kujenga umoja, haingii akilini kuwa CCM leo hawapo katika kikao hiki ni dharau ya hali ya juu waliyoionyesha nawashauri wajumbe wenzangu tusisaini mwongozi huu,” alisema Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar.
Alisema hawawezi kusaini maadili hayo hadi CCM kitakapohudhuria kwa kuwa chama hicho hakikuwa na dharura yoyote ya kukifanya kishindwe kutuma mwakilishi.
Mtumweni Jabiri kutoka Chama cha Jahazi Asilia, alisema amepata hofu kubwa ya kutowapo mwakilishi wa CCM kwa mara ya pili kwa sababu wao ndiyo wanaocheza rafu katika uchaguzi.
Mtumweni Jabiri kutoka Chama cha Jahazi Asilia, alisema amepata hofu kubwa ya kutowapo mwakilishi wa CCM kwa mara ya pili kwa sababu wao ndiyo wanaocheza rafu katika uchaguzi.
“Nadhari CCM haipo katika kikao hiki muhimu hatuna haja ya kusaini mkataba huu kwani wameonyesha dharau ya hali ya juu, sasa wataingia vipi katika uchaguzi kama wakisema hawakubaliani na maadili haya?” alihoji.
Hata hivyo, dakika za mwisho mwakilishi kutoka CCM aliwasili, hatua iliyowafanya wawakilishi wa vyama vingine kubadili muelekeo na kukubali kusaini.
Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka CUF, Omar Ali Shehe, alilitaka Jeshi la Polisi na kusaini maadili hayo.
“Lazima Jeshi la Polisi nalo lisaini mkataba huu kwani wao ndiyo wasimamizi wakuu katika kulinda amani ya nchi hasa katika uchaguzi,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ambaye pia ni Kamishna wa Zec, Nassor Khamis Mohammed, alisema Jeshi la Polisi litapelekewa waraka huo wa maadili ili kuusaini na kisha wadau wote wa vyama hivyo wataarifiwa.
Aliwataka wajumbe hao kukubaliana kusaini maadili hayo badala ya kuchukua muda mrefu wa kubishana mambo ambayo sio ya kujenga mustakabali katika kushiriki uchaguzi mkuu kwa amani na usalama.
Wajumbe walikubaliana na kuweka kando itikadi zao za kisiasa na kusaini mkataba huo.
Muongozi huo wa maadili ulisainiwa na vyama 24 vya siasa ikiwemo TLP, UDP, UMD,UPDP, NLD, NCCR-Mageuzi, ,Jahazi Asilia, DP, Demokrasia Makini, CUF, ACT -Wazalendo, ADC, AFP, APPT, CCK, CCM, NRA, Sauti ya Umma, Tadea, Chadema, Chauma na Chausta.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment