Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa akiwaonyesha wananchi mfano wa ufunguo aliokabidhi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Peoples mjini Singida jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Lowassa, Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne aliyejiondoa CCM mwishoni mwa Julai, alikuwa akizungumza na wananchi wa Manyoni mkoani Singida kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi ya Tambukareli.
Katika umati wa watu waliofurika kwenye mkutano huo, kulikuwa na mwananchi aliyebeba bango lililoandikwa “mnashangaa Lowassa kupanda daladala, mbona hamshangai twiga kupanda ndege”.
Wakati akimaliza hotuba yake, Lowassa aligeuka upande wa kushoto na akaliona bango hilo likiwa limenyanyuliwa juu. Kabla ya kulisoma alicheka, halafu akalisoma kwa sauti na kuendelea kucheka, kitu kilichowafanya wananchi waungane naye kucheka na baadaye kushangilia.
Kabla ya kuzindua kampeni zake kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi Agosti, Lowassa alifanya ziara kadhaa za kustukiza alizozielezea kuwa zililenga kufahamu matatizo ya wananchi.
Alipanda dalkadala kutoka Gongo la Mboto kwenda Chanika wilayani Ilala, kutembelea sokoni Tandale wilayani Kinondoni na Mbagala wilayani Temeke. Safari zake, ambazo zilipigwa marufuku na taasisi za Serikali, zilimsha mjadala, huku wapinzani wake wakimponda kuwa alikuwa wapi kujua matatizo ya wananchi kabla ya kugombea urais.
Twiga waliopandishwa ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na kupelekwa Arabuni waliibwa kwenye moja ya mbuga za mikoa ya kaskazini, na mtuhumiwa katika kesi hiyo alitoweka nchini na kusababisha mdhamini wake kuhukumiwa kwenda jela.
Katika mkutano wa jana, Lowassa pia alikabidhiwa funguo iliyoandikwa “Lowassa ni kiboko cha makufuli mabovu”, ujumbe unaolenga kumrushia kijembe mgombea wa CCM, Dk John Magufuli.
Kwenye mkutano huo, Lowassa alirejea wito wake wa kuwataka wananchi wanaojitokeza kwa wingi kwenye mikutano yake wahakikishe wanajitokeza kumpigia kura ili kuiondoa CCM madarakani.
“Msifurike tu kwenye mikutano, bali mnipigie kura,” alisema Lowassa ambaye alikuwa akishangiliwa wakati wote.
“Nimekuja kuwaombeni kura kila mmoja wenu anipe. Wakatalieni watakaotaka kuchukua shahada zenu. Nataka kura zaidi ya milioni 10. Mwambieni shangazi, mama, baba na hata mshikaji akapige kura na kazi ya pili iwe kuzilinda.” Mwaka 2010 watu waliojitokeza kupiga kura hawakufika milioni 9, lakini Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakadiria watu milioni 24 kujitokeza kujiandikisha kupiga kura mwaka huu. Hadi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangaza idadi ya watu waliojiandikisha.
Akizungumzia matatizo ya wananchi, Lowassa alisema kwa miaka 50 Serikali ya CCM imeshindwa kuwapa huduma bora na hivyo kilichobakia ni kuiondoa.
“Hamna maji, hampati huduma bora ya afya, kilimo bora hamna, sasa mna nini bora,” alisema Lowassa na wananchi kumjibu, “hamna kitu tunakutaka wewe utusaidie”.
Lowassa alisema Serikali atakayoiunda itakuwa ya aina yake, na ambaye hataweza kuhimili vishindo vya utendaji kazi, atakaa pembeni.
“Watu wanafurika kwenye mikutano yangu mikoani, hii inaashiria kuwa watu wanataka mabadiliko na hayo yanatakiwa kufanyika katika kura. Kama CCM wameshindwa kufanya mabadiliko kwa miaka 50 wataweza sasa,” alihoji na kuamsha shangwe kutoka kwa maelfu ya wananchi kwenye mkutano huo,
“Muungano huu (Ukawa) utaleta maajabu, wachagueni watu wetu tulete maendeleo.”
Awali, Lowassa alimuita jukwaani mgombea ubunge wa Jimbo la Manyoni Mjini kwa tiketi ya Chadema, Emmanuel Mpandagoya kueleza matatizo yanayowakabili wananchi wa Manyoni.
“Manyoni tuna tatizo kubwa la maji. Wananchi wameahidi kukupa kura, lakini ukiwa Ikulu kumbuka maji ni kero kubwa hapa,” alisema Mpandagoya akizungumzia tatizo hilo linalozungumzwa karibu katika mikutano yote.
“Pia tuna tatizo la huduma za afya, ukiwa rais, mimi mbunge wako nitakupigia simu kukukumbusha kuwa hospitali hazina dawa na baadhi ya vijiji havina zahanati.
“Tuna tatizo kubwa la walimu wa masomo ya sayansi na wengi wanaidai Serikali ya CCM na hawajalipwa madai yao. Hapa Manyoni kila kona watu wanatozwa ushuru wa bidhaa, umeme umekuwa hadithi. Hizo ndizo kero kubwa za watu wa Manyoni.”
Akieleza jinsi atakavyomaliza matatizo hayo Lowassa alisema atashughulikia tatizo la maji hadi suluhisho lipatikane.
“Nawahakikishia wakazi wa Manyoni mkinichagua, kero ya maji itakuwa historia katika wilaya yenu nitalishughulikia tatizo hili mpaka maji yapatikane, haiwezekani tangu uhuru hamna maji sasa mnafaidi nini na haya ndio maisha bora kwa kila Mtanzania?” alihoji.
Kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), takriban asilimia 80 ya watu wanaoishi mijini wanapata maji ya bomba wakati takriban asilimia 50 ya watu wanaoishi vijijini ndiyo wanaopata maji ya bomba. Inakadiriwa kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini.
Sumaye
Akizungumza kabla ya Lowassa kupanda jukwaani, Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye alisema kuwa chini ya utawala wa CCM wananchi hawapati dawa katika hospitali, akina mama wanalala chini wakati wa kujifungua, huku meno ya tembo na dawa za kulevya vikisafirishwa nje ya nchi.
“Yote hayo yanatokea, hawasemi biashara hizo ni za nani, hawa lazima waondoke,” alisema Sumaye, ambaye amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuzungumza kwenye mikutano ya Lowassa.
“Tumetoka CCM na nyinyi msiogope wanaposema kuwa nchi itaingia katika vita kama upinzani ikiingia madarakani. Lowassa ataunda Serikali itakayowajali wananchi, si vinginevyo,” alisema.
Sumaye aliwataka wananchi kutokubali kutoa kadi za kupigia kura kwa kisingizio cha kuogopa kunyanyaswa, kusisitiza kuwa safari hii watawadhibiti CCM wasiibe kura, akisisitiza kuwa ni vigumu kwa chama hicho tawala kushindana na nguvu ya umma.
Awali, mwanasheria mkuu wa Chadema na mbunge wa Singida Mashariki aliyemaliza muda wake, Tundu Lissu alisema Lowassa analipwa asilimia 80 ya mshahara wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lakini yeye na wenzake wameamua kujiondoa CCM na kupoteza stahiki zao nyingi kwa ajili ya kuwapigania wananchi.n“Sumaye na Lowassa wanahangaika na sisi ili watusaidie kuvuka kipande kidogo kilichobakia. Tunachotakiwa ni kushirikiana ili kuiondoa CCM madarakani,” alisema Lissu.
Lowassa pia alifanya mikutano Singida Mjini, Kondoa mkoani Dodoma na Ikungi ambako aliwataka wananchi kumchagua Lissu kwa mara ya pili kuwa mbunge wa jimbo la Singida Mashariki na kueleza jinsi ilani ya uchaguzi ya Chadema na Ukawa itakavyokuwa na manufaa kwa wananchi kutokana na kuwajali wakulima na wafugaji pamoja na elimu kuwa bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.
Mbunge huyo wa zamani wa Monduli leo ataendelea na mikutano mkoani Singida na kesho atakwenda Mkoa wa Shinyanga.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment