Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipofanya ziara ya kuwafariji waathirika wa upepo katika Mitaa ya Nyarugusu, Kinuni, Mwanakwerekwe na Pangawe Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa Mjini Magharibi Unguja. akimpata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Maghari Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud wakiwa eneo la tukio. .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea maeneo yaliopata maafa ya upepo katika maeneo ya Nyarugusi na maeneo mengine ya jirani.(Picha na OMPR - ZNZ)
Na Othman Khamis OMPR.
Inakadiriwa kuwa Nyumba zipatazo 77 zimeezuka mapaa na nyengine kufanya ufa kufuatia Upepo mkali uliovuma mapema leo asubuhi katika maeneo ya Mitaa ya Pangawe, Nyarugusu, Mwanakwerekwe na Kinuni ndani ya Wilaya ya Magharibi “B” Mkoa wa Mjini Magharibi.
Upepo huo umesababisha Watu Wawili kujeruhiwa katika maafa hayo ambapo Mmoja alikatwa na Bati wakati mwengine alijeruhiwa kwa kuangukiwa na Tofali wakati wa kizaa zaa hicho cha ghafla.
Mashuhuda wa tukio hilo waliviambia vyombo vya Habari kuwa upepo huo ulivuma ghafla na kutoa cheche za moto ambazo ghafla waliuona ukiezua mapaa kukata baadhi ya majengo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika katika eneo hilo ili kuwafariji na kuwapa pole Wananchi walioathirika na janga hilo lililowaacha katika mazingira magumu ya makaazi.
Akitoa Taarifa za awali ya Athari ya Upepo huo Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Serikali ya Mkoa kupitia Wilaya ya Magharibi “B” kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya Wilaya hiyo na ile ya Taifa imeanza kufanya tathmini ili kujua hasara iliyojitokeza kutokana na janga hilo.
Mh. Ayoub alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba juhudi za Serikali ya Mkoa Mjini Magharibi katika kuwahami Waathirika hao imejitolea kusaidia Kilo 25 za Mchele kwa kila Familia iliyokumbwa na janga hilo.
Mkuu huyo wa Mkoa Mjini Magharibi kupitia Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar aliwaomba wafadhili na Wafanyabiashara ndani na nje ya Nchi kusaidia janga hilo kwa lengo la kuwafariji waathirika wa Upepo huo.
Akitoa mkono wa pole pamoja na kuwafariji Wananchi hao wa Mitaa ya Pangawe na Nyarugusu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema amepata Taarifa ya tukio hilo akiwa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi na kuamua kukatisha ili kufika kuwafariji Wananchi hao.
Balozi Seif alisema hilo ni tukio lisolotegemewa kutokea ghafla kiasi hicho jambo ambalo waahtirika hao wanapaswa kuendelea kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha maafa.
Aliwahimiza Wananchi waendelee kusaidiana kama walivyoonyesha mshikamano wao wa kusaidia kwenye janga hilo jamii ibakie kuwa na utulivu na kuendelea kuishi katika maisha ya kawaida.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa Wananchi wote hapa Nchini kuwa na tahadhari na mvua zinazoendelea kunyesha kwa vile bado zitaendelea kutokea hadi mwishoni wa mwezi huu wa mei kwa Unguja Na Mwanzoni mwa Mwezi wa Juni kwa Kisiwa cha Pemba.
No comments :
Post a Comment