Edward Lowassa akiaga mwili wa marehemu Alphonce Mawazo.
Busanda. Mwili wa aliyekuwa, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo (Savimbi) umezikwa leo saa tisa alasiri kijijini kwao Chikobe Jimbo la Busanda mkoani Geita nyumbani kwa mjomba wake, huku simanzi, vilio na majonzi vikitawala.
Katika mazishi hayo, Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe alisema, ilikumuenzi Mawazo Chadema wataanzisha mfuko maalum utakao julikana kwa jina la Alphonce Mawazo Trust Fund, ili kumsadia Mtoto wa marehemu, Precious na Mama wa marehemu Hellena Gidioni,
Pia, Mbowe alisema,fedha zilizochangwa na wabunge wa Ukawa Sh33.9 milioni zitawekwa kwenye mfuko huo na michango mingine, huku akiahidi kuhuisimamia mfuko huo, ili usije kuleta mfarakano na utumike vizuri ilikumuenzi Mawazo.
Mazishi hayo yaliongozwa na Mwenyekiti huyo wa Chadema Mbowe, Mawaziri Wakuu wa wastaafu, Edward Lowassa na Federick Sumaye, wabunge wa Ukawa na viongozi waandamizi wa chama hicho.
Mwili wa Mawazo ulitolewa nyumbani kwao saa 5:51 asubuhi, na kupelekwa kwenye uwanja Chikobe uliyopo mitata chache kutoka nyumbani kwao, huku mvua kubwa ikinyesha.
Aidha Mwili wa Mawazo ulibebwa na walinzi wa Chama hicho (Red Brigade) kutoka nyumani kwao hadi kwenye viwanja hivyo ambapo ibada ya kumuombea ilifanyika kuanzia saa 6:40 mchana.
Wakati wa utoaji wa heshima za mwisho kwa mwili wa mwanasiasa huyo, idadi kubwa ya watu hasa akinamama na vijana walionekana wakipoteza fahamu, huku wengine wakilia kwa sauti kubwa.









